Wakati Katiba inayopendekezwa ikikabidhiwa kesho kwa Rais Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema hata akialikwa katika sherehe hizo hatahudhuria kutokana na majukumu aliyonayo kwa sasa.
Jaji Warioba alisema angependa kuhudhuria sherehe hiyo ambayo pia
itahudhuriwa na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wakuu wa mikoa,
mabalozi na wageni mbalimbali, lakini kutokana na dharura aliyoipata
haitawezekana.
Sherehe hiyo itafanyika mkoani Dodoma kesho na Mwenyekiti wa lililokuwa
Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta atakabidhi nakala ya Katiba
inayopendekezwa kwa Rais Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed
Shein.
Katika hafla hiyo itakayofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri, wajumbe wa
Bunge hilo walioshiriki mchakato huo kuanzia mwanzo mpaka mwisho
watapewa vyeti.
Akizungumza na gazeti hili jana, Jaji Warioba alisema hadi jana hakuwa
amepata mwaliko lakini hata kama akipewa hataweza kuhudhuria. “Siwezi
kutoka nje ya Dar es Salaam kwa siku mbili tatu hizi kwa sababu nina
dharura. Kama wakinialika nitawaomba radhi kwamba sitaweza kuhudhuria,”
alisema.
Alipoulizwa iwapo Jaji Warioba ni miongoni mwa waalikwa katika sherehe
hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi alisema angetoa majibu
leo kuhusu suala hilo lakini anaamini mkongwe huyo ni miongoni mwa
viongozi wastaafu, hivyo kualikwa ni lazima.
Sherehe yenyewe
Mkuu huyo wa mkoa alisema sherehe hizo zitatanguliwa na dua ya
kumshukuru Mungu kwa kumaliza Bunge hilo salama ambayo itafanyika leo
mchana katika Bustani ya Mwalimu Nyerere.
Wageni wengine walioalikwa ni pamoja na wakuu wa vyombo vya ulinzi na
usalama, viongozi wa dini na wengine wastaafu. “Hatuna uhakika na
viongozi wengine kutoka nje ya nchi maana mwaliko umetoka kwa muda
mfupi, lakini mabalozi waliopo nchini wote tumewaalika na makundi
mengine yote kama wakulima, wasanii, wavuvi, wafugaji na kila anayeguswa
na Katiba mwakilishi wake lazima atakuwapo,” alisema Dk Nchimbi.
Kuhusu orodha kamili ya waalikwa alisema: “Kesho (leo) naweza kuwa na
majibu mazuri kwa kila kitu maana tunashirikiana na vyombo vingine
katika kazi hii, kwa hiyo nitawaambia kwani vikao bado vinaendelea.”
Awali, Naibu Katibu wa lililokuwa Bunge la Katiba, Dk Thomas Kashililah
alisema maandalizi ya sherehe hiyo yamefanyika chini ya Ofisi ya Waziri
Mkuu
No comments:
Post a Comment