CHADEMA WAANIKA UVUNDO WA BVR; MCHEZO WA NEC, CCM NA SERIKALI


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe ameibua tuhuma nzito dhidi ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), akisema kuwa wamekaidi ushauri wa kitaalam uliowazuia wasitumie mfumo mpya wa Biometric Voter Registration (BVR) katika uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Mbowe amedai kuwa baada ya kuona zoezi la kuandikisha wapiga kura haliendi kama ilivyotakiwa, NEC walimtafuta mshauri mwelekezi aitwae Darrell Geusz, mtaalam wa masuala ya BVR kutoka Marekani ambaye baada ya kufanyia utafiti ‘hali’ ya Tanzania kuhusu mfumo huo mpya, aliwaambia wakilazimisha wanaweza kusababisha machafuko ya kisiasa nchini.
Kwa mujibu wa Mbowe, mtaalam huyo katika ripoti yake aliyoitoa mwezi Januari mwaka huu, aliiambia NEC kuwa kwa sasa Tanzania haiwezi kuandikisha wapiga kura kwa mfumo wa BVR kwa sababu ya ukosefu wa fedha, vifaa, utaalam na muda kwani mfumo huo ili uweze kufanya kazi inayotakiwa unahitaji maandalizi ya takriban mwaka mmoja.
Mwenyekiti huyo wa CHADEMA ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, ameyasema hayo jijini Mbeya wakati alipohutubia matukio mawili tofauti, akiwa katika ziara yake ya siku nne katika mikoa ya Kanda (ya CHADEMA) ya Nyanda za Juu Kusini yenye mikoa ya Mbeya, Njombe, Iringa, Ruvuma na Rukwa.
Mapema asubuhi Mwenyekiti Mbowe alihutubia wakati akifungua kikao cha Baraza la Uongozi wa CHADEMA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kisha baadae jioni akahutubia mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Dk. Slaa mjini Mbeya.
“Mshauri huyo mwelekezi ambaye ni mtaalam wa masuala ya BVR kutoka Marekani, amewahi kuisaidia nchi ya Bangladesh ambako waliandikisha wapiga kura milioni 80, aliwaambia NEC kuwa Tanzania hatuwezi kuendesha hili zoezi kwa sasa, hatuna vifaa, hatuna wataalam, hakuna muda wa kutosha, hatuna wataalam, hatuna maandalizi, akawatahadharisha wakilazimisha wanaweza kusababisha machafuko.
“Lakini katika hali ambayo haijulikani, wakiendeleza ukaidi kwa ajili ya kutaka kuibeba CCM, NEC inaonekana kutaka kuendesha zoezi hili bila kuzingatia ushauri wowote wa kitaalam wala kushirikisha wadau ambao ni vyama vya siasa wala haitaki kutoa taarifa za kutosha kwa wananchi ambao ndiyo wapiga kura wenyewe.
“NEC imekuwa ikiendesha suala hili kwa usiri usiri sana, taarifa zao wanapoamua kutoa zimekuwa za kusua sua sana, kwa kushtukiza. Tumekuwa tukidai ushirikishwaji wa kina wa shughuli na mfumo huu bila mafanikio. Tumeomba sana kupata nyaraka ili tuelewe, lakini hawataki. Wanafanya siri kubwa.
“Sasa nasi kwa sababu tunazo njia mbalimbali za kupata taarifa, tumezipata nyaraka ambazo hawataki wadau kwa maana ya vyama vya siasa tuzione.
Kwanza tumepata nyaraka ambayo inaonesha kuwa wakati walikuwa wanasema hawana kitu cha kutupatia ili tuelewe mfumo huu wa BVR, wao labda na CCM yao tangu 2013 walikuwa tayari wanajua kitakachofanyika.
“Lakini pia tumefanikiwa kupata nyaraka nyingine hii hapa. Hawa jamaa wa NEC baada ya kuzidiwa wakaamua kutafuta mshauri mtaalam kutoka Marekani ambaye anasifika duniani, yaani katika masuala ya BVR ni authority, ameandika ripoti yake yenye kurasa 16, amewapatia hadi ushauri wa tahadhari ya madhara ya kiusalama jamaa wa NEC na Serikali ya CCM hawataki kusikia,” amesema Mbowe.
Mbowe ameongeza kusema kuwa wakati mshauri huyo mtaalam wa BVR akiwatahadharisha NEC kuhusu muda, tume imeendelea kusema kuwa zoezi hilo litafanyika na kufanikiwa kwa kipindi cha ndani ya miezi miwili, jambo ambalo Mwenyekiti wa CHADEMA amesema kuwa serikali inacheza na ‘roho ya amani katika nchi’.
Alisema kuwa mazingira yanayoendelea nchini Tanzania katika suala la mchakato wa hatua mbalimbali za uchaguzi mkuu wa mwaka huu, yanatengeneza hali ya kutokuaminiana miongoni mwa wadau, akisema kuwa hali hii husababisha uchakachuaji na katika nchi zingine imesababisha machafuko ya kisiasa.

No comments: