Askari hao wanaokisiwa kufikia saba, wakiwa na silaha nzito katika gari la wazi waliwasili nyumbani kwa Mbowe majira ya saa saba na nusu usiku na kuwaamuru askari wanaolinda nyumbani kwake kumtoa Mbowe nje ili waonane naye.
Walinzi wa Mbowe walihoji uhalali wa ukamataji huo na kuwataka polisi wawaoneshe hati ya kumkamata, lakini hawakuweza kuionesha, hali iliyozusha wasiwasi kwa walinzi wa kiongozi huyo.
Hata hivyo walinzi hao waliwaambia polisi hao kuwa Mbowe ambaye pia ni kiongozi mkuu wa kambi ya upinzani bungeni alikuwa safarini, jibu ambalo lilipokewa kwa shingo upande na askari hao.
Polisi hao baada ya kuona wameshindwa kukamilisha kazi hiyo, waliwaachia walinzi hao namba ya simu 0754-085600 ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Ernest Kimola, wakiwaagiza kuhakikisha wanamwambia Mbowe awasiliane na kamanda huyo.
RCO amsukumia RPC, akana
Hata hivyo, alipohojiwa na Tanzania Daima Jumapili kwa njia ya simu, Mkuu wa Upelelezi Kimola aligoma kuzunguzia suala hilo na kumtaka mwandishi kuwasiliana na mkuu wake wa kazi, ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamilius Wambura, akidai ndiye mwenye haki ya kutoa ufafanuzi wa jambo hilo.
“Unajua mimi si msemaji wa polisi, wasiliana na kamanda wa mkoa, maana ndiye mwenye uwezo wa kutoa maelezo,” alisema Kimola na kukata simu. Lakini alipopigiwa simu Kamanda Wambura aliruka kimanga, kwa mshangao, akidai kutojua lolote kuhusiana na polisi kuvamia nyumbani kwa Mbowe.
“Kwa kweli ndiyo napata taarifa hizo kutoka kwako, kuwa kiongozi huyo alifuatwa na polisi, maana silijui suala hilo hata kidogo,” alisema Wambura, naye kama alivyofanya Kimola akakata simu.
Kauli ya CHADEMA
Lakini wakati Kimola akikataa kusema chochote, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema kuwa alizungumza kwa njia ya simu na Kimola kuhusiana na kitendo cha polisi kuvamia nyumbani kwa kiongozi huyo wa juu wa kisiasa, na kudai kupewa majibu ya kushangaza.
Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika Manzese, Wilaya ya Kinondoni, Dk. Slaa alisema Kimola alijitetea akidai kwanza kukana kufika nyumbani kwa Mbowe usiku wa manane. Pili, alisema kuwa hawakwenda kumkamata Mbowe, isipokuwa kufanya naye mazungumzo na kisha wangemwacha.
Slaa alisema kitendo hicho kimewashitua na ni cha kinyama na kilichokiuka sheria za nchi na haki za binadamu. Aliongeza kwamba, daima wamekuwa wakilishutumu Jeshi la Polisi kwa kutumika vibaya kukandamiza wapinzani, lakini mara zote CHADEMA kimepuuzwa na sasa jeshi hilo limeamua kuvamia makazi ya viongozi wa kisiasa kwa madhumuni yasiyoeleweka.
Alisema haijulikani nini kingetokea ikiwa Mbowe angekuwa ndani, ikiwa walinzi wangeamua kugoma kumwachia kiongozi wao. “Tuna hofu kubwa na usalama wetu, maana pale wangeweza kufanya lolote, hata kumuua na kisha kutoa matamshi kuwa walikuwa wanajibishana kwa risasi, kama ambavyo imekuwa jadi ya askari polisi kutoa taarifa za uongo na upotoshaji wanapoua watu,” alisema Slaa.
Alisema ikiwa polisi walikuwa na shida ya kweli, wangemwita kwa njia sahihi na si kumvamia na kuingilia uhuru wake na wa familia yake kama wanakamata gaidi ama jambazi hatari.
Dk. Slaa alisema Mbowe anayo ofisi inayojulikana, na kama kweli hakukuwa na jambo baya lililopangwa na polisi hao wasingeweza kufanya uhuni kama walioufanya.
“Kama wanaweza kuvamia nyumbani kwa kiongozi mkubwa kama Mbowe wakiwa na silaha nzito, itakuwaje kwa viongozi wa kawaida na raia?” alihoji Slaa.
Kutokana na tukio hilo la kuogofya, CHADEMA imemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwaeleza Watanzania maana ya matukio haya ambayo yamedhamiria kuleta vurugu kubwa nchini. Kadhalika, wamemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema, kuueleza umma kile kilichokusudiwa na askari wake kuvamia nyumbani kwa Mbowe mithiri ya jambazi.
Itakumbukwa pia kuwa hivi karibuni askari polisi wa Mkoa wa Arusha walivamia nyumbani kwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, wakiwa na silaha nzito na mbwa, na kumkamata, kisha kumtupa rumande kwa siku nzima.