Kwa niaba ya baraza la uongozi la mkoa wa Arusha, napenda kuujulisha umma wote kwa ujumla kuwa mwenyekiti
wa wilaya ya monduli Mchungaji Amani Silanga Mollel amekoma/amesimamishwa kuwa
Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya monduli kuanzia tarehe 29 Novemba 2013 kufuatia
tuhuma nzito za uvunjifu wa kanuni za maadili ya chama.
Hatua hii imefikiwa baada ya kuthibitika na yeyé mwenyewe
kukiri mbele ya kikao cha kamati tendaji ya wilaya ya monduli kilichoketi
tarehe 29 Novemba 2913 saa NNE asubuhi kuwa alitoa tamko batili akitumia
wadhifa wa mwenyekiti wa wilaya bila ridhaa ya kamati tendaji na huku
akidanganya kuwa ni tamko kwa niaba ya wilaya ya monduli.
Katika tamko lake ametoa tuhuma dhidi ya wajumbe wa
kamati kuu na viongozi wakuu wa kitaifa kwa maamuzi halali ya kikao cha kamati
kuu huku akijua kuwa anavunja kanuni za chama kwa mujibu wa katiba ya chama
toleo la mwaka 2006 ya Kanuni za uendeshaji kazi za chama, sura ya KUMI, ibara ya
10 (X) “Kiongozi asitoe tuhuma zozote
juu ya viongozi wenzake pasipo kupitia vikao halali na kuzingatia taratibu na
ngazi zilizoelezwa kwenye kanuni za chama”.
Sambamba
na hilo, Mchungaji Amani Silanga ametoa tuhuma za uzushi, uongo na upotoshaji na
kutaka kuaminisha jamii kuwa chadema ina makundi ya CHADEMA Asili na CHADEMA
Family kitu ambacho ni upotoshaji mkubwa na wa hatari kwa ustawi na umoja wa
chama na kinyume na kanuni za uendeshaji kazi za chama, sura ya KUMI, ibara ya 10
(VII), “Kiongozi anatakiwa kuwa mkweli
na muwazi wakati wote hususani katika vikao halali na aachane na vikundi vya
majungu, wadanganyifu (Rumour Mongers). Ni mwiko kwa kiongozi kujihusisha na
upotoshaji wa maamuzi wa vikao halali”. Kamati tendaji ya wilaya ilipomtaka
aonyeshe CHADEMA asili ni kina nani na CHADEMA family ni kina nani alishindwa
kutoa maelezo yoyote ya maana na kufikia hatua ya kutaka kuvuruga kikao kwa kuleta
vijana wahuni wapatao 17 ndani ya kikao ambao wengi walijulikana kuwa sio WANACHADEMA.
Katika utambulisho wake wa majigambo Mchungaji Amani SIlanga kwa kiburi na
kejeli amejitambulisha na kukiri kuwa yeye yupo kambi ya Zito Kabwe na hakuna
wa kumfanya kitu maana ni mjumbe wa baraza kuu la chama. Maneno yake
yalidhihirisha kuwa Mchungaji Amani Silanga anashiriki mpango wa kuunda makundi
yasiyo na tija ndani ya chama na hivyo kuwa kinyume na sura
hiyo hiyo ya kumi ya kanuni za uendeshaji kazi za chama ibara ya 10 (IX), “Kiongozi asijihusishe au kushiriki na
vikundi au vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa
chama au wanachama wake”.
AZIMIO LA BARAZA
LA UONGOZI LA MKOA WA ARUSHA:
Baraza la uongozi la mkoa lililoketi tarehe 29 Novemba
2013, limepokea mapendekezo ya kamati tendaji ya wilaya na kuzingatia hofu
kubwa iliyoainishwa na kamati tendaji kufuatia matendo mengi yanayotia shaka ya
uadilifu na uwezo wa kiuongozi wa Mchungaji Amani Silanga na hivyo baraza la
uongozi la mkoa limeridhia kuwa amevunja kanuni za maadili ya chama sura ya
KUMI ibara ya (VII) hadi (XII) na hivyo kupelekea ukomo wa yeye kuwa Mwenyekiti
wa wilaya kuanzia tarehe 29 Novemba 2013. Baraza la mkoa likiwa mamlaka ya
nidhamu kwa mujibu wa katiba ibara ya 6.3.6 (a) (iv) limemjulisha tuhuma zake
na hatua hii stahiki iliyochukuliwa. Kwa vile Mchungaji Amani Silanga alikiri
kosa hili mbele ya kamati tendaji ya wilaya bila kulijutia au kuomba msamaha,
baraza la mkoa limechukua hatua hii stahiki kwa maslahi ya chama na kuwa
uchunguzi zaidi utafanyika ili kufikia maamuzi makubwa zaidi ya tuhuma nyingi kwa
mujibu wa kanuni za hatua za kinidhamu.
Baraza la uongozi la mkoa wa Arusha, linatoa onyo kwa
wote ambao wapo katika mtandao huu mchafu, ama watoke wenyewe mapema maana hawatavumiliwa
kamwe. Baraza la uongozi wa mkoa liliona kuwa Mchungaji Silanga amepotoka na
hivyo yeyé kuendelea kuwepo ndani ya chama wakati wa uchunguzi wa tuhuma hizi
nzito dhidi yake ni hatari zaidi kwa ustawi wa chama na hivyo baraza likaridhia
kwa kuzingatia tafsiri ya katiba ya chama ibara ya 6.3.4 (c) wa yeyé kukoma
uongozi na hivyo akae nje kwa muda na waliopotoka wenzake.
Amani Golugwa
Katibu wa
CHADEMA – Mkoa wa Arusha.
(Kwa niaba ya Baraza
la Uongozi la Mkoa wa Arusha)
Tarehe 30
Novemba 2013