SERIKALI YA TANZANIA ICHUKUE HATUA ZA HARAKA KUNUSURU WATANZANIA WAISHIO AFRIKA KUSINI DHIDI YA GHASIA NCHINI HUMO

KURUGENZI YA MAMBO YA NJE 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


SERIKALI YA TANZANIA ICHUKUE HATUA ZA HARAKA KUNUSURU WATANZANIA WAISHIO AFRIKA KUSINI DHIDI YA GHASIA NCHINI HUMO

Kumekuwepo na hali ya raia wa Afrika Kusini kushambulia , kujeruhi na kuua raia wa kigeni wa Kiafrika wanaoishi nchini Afrika Kusini.

Hali hii inadaiwa kuchochewa na ukosefu mkubwa wa ajira kwa wananchi wa Afrika Kusini wanaodai ajira hizo kuchukuliwa na Waafrika wa mataifa mengine na hivyo wao wenyeji kubakia kwenye dimbwi kuu la umasikini.

Ni mtazamo wa kuimarika kwa kiwango cha umasikini kwa wananchi wengi nchini humo dhidi ya kuimarika kwa kiwango cha utajiri kwa wachache kunakopelekea ghasia hizi

Zaidi, mali za Waafrika wageni nchini humo zimekuwa zikiharibiwa baada ya wamiliki kukoswa katika mashambulizi hayo.

Aidha, kama nchi nyingine za Kiafrika, Tanzania ina idadi kubwa ya raia wake wanaoishi nakufanya kazi nchini Afrika Kusini. Na mpaka sasa inadaiwa kuwa watanzania wawili (2) wameuwawa katika ghasia hizo za wenyeji dhidi ya Waafrika wageni.

Kwa misingi hiyo:

1. CHADEMA inalaani vikali hali ya raia kudhuru na kutwaa uhai wa raia yoyote yule. CHADEMA kama muumini wa haki za binadamu inayojumuisha haki kuu ya kuishi inasikitishwa na hali hiyo ya machafuko inayoondoa usalama wa sio tu kwa raia wa kigeni wa Kiafrika walioko Afrika Kusini bali pia kwa raia wengine wa Afrika Kusini ambao hawawezi kufanya shughuli zao kwa ukosefu wa usalama nchini humo.


CHADEMA inawasii raia wa Afrika Kusini kuwachukulia Waafrika wenzao kutoka mataifa mengine kama ndugu zao ambao kwapamoja walishrikiana kupambana na ubaguzi wa rangi na hatimaye kuleta uhuru kwa taifa hilo. Ni muhimu raia wa Afrika Kusini wakatatua matatizo yao ya ndani hasa ya kiuchumi kwa kushirikina na wenzao wa mataifa ya Afrika waishio nchini humo na si kuwaona kama maadui zao.

2. CHADEMA inaitaka serikali ya Tanzania ishirikiane na serikali ya Afrika Kusini kuchukua hatua za haraka kunusuru maisha ya watanzania waishio nchini Afrika Kusini dhidi ya ghasia hizi kwa kuwahakikishia usalama wao ama kuwawekea utaratibu wa kuondoka ama nchini humo na kurejea nyumbani ama kwenye miji yenye machafuko kama Durban na kuwapeleka kwenye miji ya usalama zaidi mpaka hali itakapotengamaa kwenye miji hiyo kama ilivyofanya kwa Watanzania waishio Yemen ambako nako machafuko yamekithiri. Ni muhimu Serikali ikawa makini kwa jambo hili kwani teyari mataifa mengine ya kiafrika ya Botswana, Malawi na Zimbabwe yaneshaanza kuwaondoa raia wake nchini humo kwa kuhofia usalama wao.

3. CHADEMA inazikumbusha nchi za Kiafrika ambazo zina utajiri mkubwa wa rasilimali kuhakikisha inatatua matatizo ya kiuchumi yanayozikabili nchi hizo ikiwa ni pamoja na kupunguza tofauti ya kipato kati ya wengi wasio nacho na wachache wenye nacho.

Ni muhimu serikali hizi kujikita katika kupambana na umasikini kwa kutengeneza fursa za ajira kwa raia wake na hivyo kupunguza kiwango cha umasikini na hatimaye kuondoa mazingira ya machafuko yanayosababishwa na hasira za wananchi kutokana na hali yao ya umasikini.

Kwa mantiki hiyo, ni muhimu Jumuiya za kikanda na Umoja wa Afrika wenyewe (AU) zikaweka msisitizo wa ukombozi wa kiuchumi unawaweza kukidhi haja na matakwa ya raia wa bara hili.

4. Kipekee, CHADEMA inaikumbusha serikali ya Tanzania kuichukilia hali ya Afrika Kusini kama taadhari kwake kwani hali ya umasikini na ukosefu wa ajira hapa nchini imekuwa kubwa kiasi cha kuibuka kwa vikundi vya kihalifu vya Komando Yoso na Panya Road vilivyofanya mashambulizi na uporaji kwa raia wengine. Tofauti ndogo iliyopo kati ya Afrika Kusini na Tanzania ni kwamba Afrika Kusini raia wazalendo wanashambulia waafrika wa mataifa mengine wakati hapa Tanzania ilikuwa ni kushambuliana baina ya Watanzania.

Imetolewa leo tarehe 18.04.2015 Jijini Dar es salaam na;
Deogratias Munishi
Mkuu wa Mambo ya Nje – CHADEMA
+255715887712

No comments: