CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
CCM WAMEDHIHIRISHA FIKRA ZA KIKABURU
Katika hali isiyokuwa ya kawaida ambayo kwa namna yoyote
haiwezi isingeachwa imee katika fikra za watu achilia mbali kuachiwa
itembezwe hadharani, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia katika mojawapo
ya mabango yaliyobebwa na wanachama wake kuiadhimisha Sikukuu ya
Mapinduzi ya Zanzibar, imedhihirisha kuwa inakumbatia fikra hatari za
kikaburu.
Kupitia bango hilo ambalo kwa namna lilivyotengenezwa na
lilivyobebwa ni vigumu kuamini kuwa liliibuka ghafla kama vile kitambaa
cha mfukoni, mwanachama wa CCM akiwa amesindikizwa na wenzake, waliopita
mlangoni mwa Uwanja wa Amani bila kuzuiliwa, kukemewa wala kubugudhiwa,
ujumbe hatari wa kibaguzi umeandikwa 'MACHOTARA HIZBU ZANZIBAR NI NCHI
YA WAAFRIKA'. Hizi ni fikra za kikaburu. Ni ishara ya mbegu za kibaguzi
zilizokomaa na sasa zinachipua.
Kwa wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa nchini na kipekee
katika muktadha huu, siasa za Zanzibar wataelewa kuwa kauli iliyotolewa
katika bango hilo, si ya bahati mbaya. Ni matokeo ya siasa za chuki
zinazopaliliwa, kusimamiwa, kuratibiwa na hata kunyamaziwa na uongozi wa
juu kabisa wa CCM.
Tutatoa mfano. Moja ya maskani maarufu za masuala ya
kisiasa Visiwani Zanzibar inayomilikiwa na CCM iitwayo Kisonge imekuwa
na kawaida ya kuandika lugha hatari zinazoashiria ubaguzi ulio wazi
kabisa ulio na maudhui sawa sawa na huu uliotolewa leo kwenye Sikukuu ya
Mapinduzi.
Mojawapo ya kauli ambazo ziliandikwa katika ubao ulioko
katika maskani hiyo hivi karibuni wakati wa joto la Uchaguzi Mkuu
uliopita, iliandikwa hivi "Katiba ni ya Unguja na nyinyi Wapemba mwende
mkatengeze yenu Pemba."
Lugha hiyo na nyingine za namna hiyo kama ilivyotokea leo,
zimekuwa zikitolewa mbele ya viongozi wa CCM au wanaziona lakini kwa
sababu wanazozijua wao, pengine zinawasaidia katika kufikia malengo ya
siasa hatarishi zinazokiuka misingi yote ya demokrasia, zimekuwa
zikifumbiwa macho na kuzidi kumea vichwani mwa wanachama wao na kuleta
mpasuko wa ubaguzi wa itikadi za kisiasa, rangi, kanda, kabila na hata
dini, si Zanzibar pekee bali nchi nzima.
Kilichotokea leo Zanzibar, ni mwendelezo usiokuwa wa bahati
mbaya bali maelekezo ya kimkakati ya kueneza propaganda za chuki
miongoni mwa Watanzania ambayo ndiyo imebakia kuwa silaha pekee ya
kuibeba CCM ikiwa ni dalili ya wazi ya chama kilichofilisika sera,
kuacha misingi yake, kuishiwa ushawishi wa hoja na kukosa uhalali wa
kisiasa hivyo kujihalalisha kwa ubaguzi kama huo.
Ni mwendelezo wa kauli za viongozi wakuu wa chama hicho
ambazo hutolewa hadharani kwenye majukwaa ya siasa, wakiwabagua
wanachama, wapenzi, wafuasi wa vyama vingine kuwa ni wa dini fulani,
kanda fulani au kabila fulani. Wakijua kabisa hakuna kikundi chochote
cha kisiasa chenye sifa hizo kwa sababu ni kinyume cha sheria na misingi
ya taifa letu.
Ni mwendelezo wa kauli iliyowahi kutolewa na viongozi wa
chama hicho dhidi ya viongozi wenzao na wala viongozi wakuu wa CCM
hawakuthubutu hata kukaripia, tena yakiwa maazimio rasmi ya kikao kwamba
"Rais wa Tanzania hawezi kutoka Kaskazini".
Kauli hiyo iliyotolewa baada ya kikao ilikuwa kauli ya kikaburu sawa sawa kabisa na ile iliyotolewa leo huko Zanzibar.
Mwalimu Nyerere, Baba wa Taifa aliwahi kusema ukaburu si rangi, ni fikra.
CHADEMA tunalaani na kupinga kwa nguvu zote mipango,
mikakati, tabia na chembechembe za ubaguzi wa aina yoyote, ukiwemo huu
wa kisiasa ambao sasa unaanza kusakafiwa kwa ubaguzi wa rangi kwa sababu
tunaamini wanaobeba agenda hii hawataishia hapo bali watazidi kutugawa
Watanzania pia kwa ubaguzi wa ukanda, ukabila na udini kama ambavyo
wamekuwa wakijaribu kuchochea.
CHADEMA kwa kusimamia misingi yake na kuzingatia kikamilifu
misingi ya taifa letu hasa haki, uadilifu, utu, umoja na uzalendo,
haiko tayari kuona taifa likifikishwa huko na kuhatarisha maisha ya
jamii nzima ya Watanzania kwa sababu ya maslahi ya kikundi cha watu
wachache.
Tunamkumbusha Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Ernest Mangu
kuwa kauli za namna hii ambazo zimekuwa zikipaliliwa na viongozi wa CCM
na wengine wakitumia nafasi za kiserikali kuchochea ubaguzi ambao ni
hatari kwa amani ya nchi na usalama wa raia na mali zao, ni ushahidi wa
wazi kwa ajili ya hatua za kisheria badala ya jeshi hilo kujikita katika
kubambikia wanachama, wafuasi na wapenzi wa vyama vya upinzani, hususan
UKAWA tuhuma na kesi zisizokuwa msingi wowote kwa maslahi tu ya kisiasa
kuisaidia CCM.
Wakati tukimtaka Rais John Magufuli kutimiza kwa vitendo
kauli yake ya kwamba Serikali yake haitawabagua watu kwa misingi ya
kisiasa (huku Waziri Mkuu wake akitoa maagizo kinyume kabisa na kauli
hiyo) tunakitaka CCM, kupitia kwa Mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete kama
hakiko nyuma ya agenda hizo za kibaguzi na fikra hizo za kikaburu,
kichukue hatua za haraka mara moja kuwawajibisha viongozi wake
waliosimamia na kuachia jambo lililotokea leo huko Zanzibar.
Imetolewa leo Jumanne, Januari 12, 2016 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Habari
CHADEMA
CHADEMA
No comments:
Post a Comment