MBUNGE WA SAME (M) CHADEMA AFANIKIWA KUREJESHA GARI LA WAGONJWA LILILOPELEKWA TEMESA MIEZI 6

HOFU ya vifo vya wanawake wajawazito na watoto katika kata ya Ndungu wilayani Same, imetoweka baada ya mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Naghenjwa Kaboyoka kurejesha gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya Ndungu ambalo liliondolewa kwa madai ya kufanyiwa ukarabati.

Kituo hicho cha afya hakikuwa na gari hilo kwa zaidi ya miezi tisa, jambo ambalo lilitishia maisha ya wananchi waishio kata hiyo na maeneo jirani. Uwepo wa gari hilo husaidia wananchi katika utoaji wa huduma za haraka kwenda katika hospitali ya wilaya ama ile ya rufaa ya KCMC kulingana na dharura zinazojitokeza.

Akizungumza na gazeti hili, Kaboyoka alisema kabla ya kuwa mbunge alipata malalamiko ya wananchi kwamba hawana uhakika wa gari la wagonjwa litakalowawezesha kwenda hospitali za wilaya na rufaa baada ya gari lao kuondolewa na kupelekwa kusikojulikana.

“Nilifuatilia na kupewa taarifa kuwa gari limepelekwa kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa). Hili jambo halikuniingia akilini, nilifuatilia na baadaye gari lilirejeshwa katika kituo na sasa utoaji wa huduma za dharura zimerejea,” alisema.

Kadhalika mbunge huyo alisema mipango mingine aliyoa nayo ni kulitoa gari la wagonjwa lililopelekwa kisiasa kata ya Kilangare kwenda Kituo cha Afya Vunta ili lisaidie kundi kubwa la jamii ikilinganishwa na mahali lilipo sasa na tayari Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ameridhia mpango huo.

Alisema ameanza mchakato wa kuiombea kibali Hospitali ya Bombo iliyopo Gonja inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kuwa hospitali teule ya wilaya hiyo.

No comments: