MAAZIMIO YA KAMATI KUU YA CHADEMA


Baada ya majadiliano Kamati Kuu imeazimia ifuatavyo;
3.1 Septemba 1, siku ya mikutano ya hadhara nchi nzima
Kamati kuu imeagiza ngazi zote za chama kuanzia ngazi ya msingi, Kata, Majimbo, Wilaya, Mikoa, Kanda, Mabaraza na Taifa kukaa vikao vyake vya kikatiba na imeelekeza ajenda ya vikao hivyo kuwa ni kujadili hali ya siasa, hali ya uchumi na maandalizi ya mikutano ya hadhara ya tarehe 01 Septemba, 2016 nchi nzima.
3.2 Wanasheria wa Chama kuchukua hatua
Kamati Kuu imewataka wanasheria wa chama kukaa na kuyatazama mambo yote ambayo yametokea na kuchukua hatua za kisheria kwa lengo la kuyatafutia suluhisho la kisheria.
3.3 OPERESHENI UKUTA
UMOJA WA KUPAMBANA NA UDIKTETA TANZANIA (UKUTA)
UTANGULIZI
Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika utangulizi kuna maneno yameandikwa na ambayo yamekaziwa na sheria namba 15 ya mwaka 1984 ibara ya 3 na sheria namba 1 ya mwaka 2005 ibara ya 3. Katika utangulizi huo wa katiba yetu imeandikwa kama ifuatayavyo;
“KWA KUWA Sisi wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani”
“NA KWA KUWA misingi hiyo yaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye demokrasia, ambayo Serikali yake husimamiwa na Bunge lenye wajumbe waliochaguliwa na linalowawakilisha wananchi na pia yenye Mahakama huru zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila woga wala upendeleo wowote na hivyo kuhakikisha kwamba haki zote za binadamu zinadumishwa na kulindwa na wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa uaminifu:”
“KWA HIYO, BASI, KATIBA HII IMETUNGWA NA BUNGE MAALUM LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA kwa niaba ya Wananchi kwa madhumuni ya kujenga jamii kama hiyo na pia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Tanzania inaongozwa na Serikali yenye kufuata misingi ya Demokrasia ujamaa na isiyokuwa na Dini”
Aidha kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzana ibara ya 3 (1) inasema kuwa “Jamhuri ya Muungano ni Nchi ya Kidemokrasia na ya kijamaa, isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa”
Ni wazi sasa kuwa kuna tishio kubwa dhidi ya ukuaji wa Demokrasia hapa Nchini mwetu kutoka kwa viongozi wa serikali hii ya awamu ya tano kukandamiza Demokrasia na madhara ya kukandamizwa kwa demokrasia yameshaanza kulitafuna taifa letu.
Ni dhahiri kuwa kama raia wema tuna wajibu na haki ya kuilinda na kuitetea Katiba ya Nchi na kuhakikisha kuwa haivunji na yeyote na misingi ya Kidemokrasia ambayo ilijengwa kwa miongo mingi inaendelea kuimarika, kulelewa na kukuzwa mara dufu.
3. 4 KWANINI UKUTA NI MUHIMU !
Wakati wa Ufashisti wa Adolf Hitler huko Ujerumani unaanza kuchipua kabla ya kukomaa alianza kuchukua hatua mbalimbali za kuwanyamazisha Wajerumani kwa njia mbalimbali ili aweze kutawala kwa mkono wa Chuma.
Alikuwepo Mchungaji mmoja anayejulikana kwa jina la Martin Niemoller na ambaye alikuwa akimsemea Hitler kwa kila hatua ambazo alikuwa anachukua dhidi ya makundi mengine katika jamii ya wajerumani bila kujua kuwa lilikuwa ni suala la muda tu kabla hata yeye hajafikiwa na mkono wa Chuma wa Hitler.
Mchungaji huyu ni maarufu sana kwa msemo wake ambao aliutoa alipofikiwa na mkono wa Hitler ambao ulimpelekea kuishia jela kwa miaka 7 na wakati huo hapakuwa na mtetezi wa kumsemea, alisema hivi;
First they came for the Socialists, and I did not speak out—
Because I was not a Socialist.
Then they came for the Trade Unionists, and I did not speak out—
Because I was not a Trade Unionist.
Then they came for the Jews, and I did not speak out—
Because I was not a Jew.
Then they came for me—and there was no one left to speak for me.
3.5 HALI TANZANIA IKOJE?
Tangu utawala wa awamu ya Tano ulipoingia madarakani mwezi Novemba, 2015 umechukua hatua mbalimbali za kubinya Demokrasia na kuua dhana ya utawala bora kwa njia mbalimbali.
Yapo makundi ya kijamii ambayo tayari yameshaumizwa au kubinywa na watanzania walio wengi wanakaa kimya kwa sababu wao sio sehemu ya kundi husika ambalo limenyimwa haki au kwa kuwa hajafikiwa moja kwa moja.
3.6 KWANINI NI MUHIMU KUJENGA UKUTA.
• Rais alipiga marufuku safari za nje kwa watumishi wa umma- sikusema kwa kuwa mimi sikuwa mtumishi wa umma
• Rais aliitaka mahakama kuu iwahukumu wafanyabiashara ambao wana kesi za kodi na serikali lazima ishinde-sikusema kwa kuwa sikuwa mfanyabiashara na wala sikuwa na kesi ya kodi
• Serikali iliingilia Bunge na kupanga kamati za kudumu za Bunge-sikusema kwa kuwa mimi sikuwa mjumbe
• Serikali ilizuia matangazo ya Bunge live-sikusema kwa kuwa mimi sio Mbunge
• Wabunge wa Upinzani kunyanyaswa Bungeni na kuonewa –sikusema kwa kuwa mimi sio UKAWA
• Hotuba za Upinzani kufutwa Bungeni kinyume cha Kanuni za Bunge –sikuwa mpinzani nilikaa kimya
• Bunge kurejesha fedha zake kwa Rais kinyume cha sheria –sikusema kwa kuwa halinihusu
• Tume ya Taifa ya Uchaguzi kurejesha fedha kwa Rais kinyume cha sheria –sikusema kwa kuwa Tume hainihusu
• Serikali Kuwafukuza na kuwadhalilisha wanafunzi wa UDOM –sikusema kwa kuwa sina ndugu wala mtoto anayesoma UDOM.
• Mikutano ya kisiasa kupigwa Marufuku –sikusema kwa kuwa mimi sio mwanasiasa
• Wafanyabiashara kupelekewa bili kubwa za kodi na hata kuzuiliwa kwa Akaunti zao-sikusema kwa kuwa mimi sio mfanyabiashara
• Uchumi unaporomoka kwenye sekta zote nchini -sikusema kwa kuwa mimi sijawahi kumiliki uchumi
• Fao la kujitoa limeondolewa kwenye Mifuko ya hifadhi ya jamii, sikusema kwa sababu mimi si mwanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii.
• Mashirika na Makampuni kuanza kupunguza wafanyakazi kutokana na kuporomoka kwa uchumi –sikusema kwa kuwa sijapunguzwa kazini
• Mabalozi na wanadiplomasia kuzuiliwa kukutana na viongozi wa kisiasa bila kibali cha serikali- sikusema kwa kuwa halinihusu
• Watumishi wa umma kulazimishwa kwenda kinyume na sheria na kanuni za utumishi wa umma wametakiwa kuwa Makada wa CCM –sikusema kwa kuwa mimi sio mtumishi wa umma
• Ukaguzi wa vyeti vya kidato cha nne na kutumika kama msingi wa kufukuza watu kazi hata kama ni Maprofesa –sikusema kwa kuwa hawajaja kwenye sekta yangu
• Watumishi wa umma kutumbuliwa majipu bila kufuatwa kwa sheria na kanuni za utumishi wa umma –sikusema kwa kuwa mimi sikutumbuliwa
• Mawakili kuunganishwa kwenye kesi za wateja wao wanapoenda kuwatetea –sikusema kwa kuwa mimi sio wakili
• Waalimu kukatwa mishahara iwapo dawati litavunjika kwenye shule yake –sikusema kwa kuwa mimi sio mwalimu
• Kupotezwa kwa wana CCM ambao watapinga kauli ya Mwenyekiti au kuwa na maoni tofauti-sikusema kwa kuwa mimi sio mjumbe wa vikao vya CCM .
• Muswada wa sheria ya haki ya kupata habari na adhabu ya kifungo cha miaka 15-20- sikusema kwa kuwa mimi sio mwandishi wa habari
• Viongozi wa dini kudhalilishwa –sikusema kwa kuwa mimi sio kiongozi wa dini
• Unyanyasaji na udhalilishaji wa wananchi Zanzibar –sikusema kwa kuwa mimi sio mzanzibari
3.7 TUCHUKUE HATUA!
i. Kwa kuwa wewe tayari umeshafikiwa hauna budi kujenga UKUTA ili kuzuia wengine wasidhurike na utawala huu.
ii. Kwa kuwa wewe hujafikiwa na ndio maana husemi wenzako wanapofikiwa, njoo tujenge UKUTA ili ukifikiwa awepo wa kusema
iii. Tuungane Tujenge UKUTA ili kuzuia uchumi wetu kuporomoka
iv. Njoo Tujenge UKUTA kuzuia Udikteta huu
v. Tujenge UKUTA tuilinde Katiba yetu
vi. UKUTA huu ni wa wananchi wote bila kujali dini, kabila, chama cha siasa au rangi
Historia inaonyesha kuwa Duniani pote Hakuna utawala uliwahi kuushinda UKUTA wa wananchi .Na hii ndio Nguvu ya Umma. Kila mmoja achukue hatua popote alipo ya kujenga UKUTA!


Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Mh Freema A. Mbowe Akiongea na wanahabari kuhusu Operation UKUTA

Katibu wa CHADEMA Taifa Mh Vicent Mashinji

No comments: