MAELEZO JUU YA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

1. Msimamizi wa Uchaguzi atamteua Afisa wa Umma ambaye ataandikisha na kuandaa orodha ya wapiga kura katika Kitongoji kwa ajili ya uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji siku ishirini na moja kabla ya siku ya uchaguzi.

2. Watendaji wa vijiji, Mitaa na Kata hawataruhusiwa kuandikisha na kuandaa orodha ya wapiga kura.

3. Uandikishajhi wa Orodha wa Wapiga kura utafanyika kwenye majengo ya umma na pale ambapo hakuna jengo la umma, uandikishaji utafanyika kwenye sehemu ambayo Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi atakuwa amekubaliana na Viongozi wa Vyama vya Siasa.

4. Vituo vya uandikishaji wa orodha ya wapiga kura vitafunguliwa kuanzia saa moja na nusu asubuhi na kufungwa saa kumi jioni.

5. Vyama vya siasa vitaruhusiwa kuwepo wakati wa uandikishaji wa wapiga kura.

6. Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi atabandika mahali pa matangazo ya uchaguzi Orodha ya wapiga kura na kutunza kumbukumbu yake.

7. Mkazi yeyote wa Kitongoji au vyama vya siasa vitakuwa na haki ya kukagua Orodha ya wapiga kura katika muda wa siku nne tangu tarehe Orodha ya wapigakura ilipobandikwa mahali pa matangazo ya uchaguzi ili kutoa pingamizi au maoni ya usahihi wa orodha hiyo na anaweza kuomba-
(a) Orodha irekebishwe kwa kuongeza jina lake au jina la mkazi; au
(b) orodha irekebishwe kwa kufuata jina lililoorodhoshwa kwa vile aliyeoorodheshwa hana sifa ya kupiga kura katika Kitongoji husika.

8. Pingamizi dhidi ya mtu kuandikishwa kuwa mpiga kura litawasilishwa kwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi ambaye atalitolea uamuzi na kurekebisha orodha ya wapiga kura iliyotangazwa katika muda wa siku tano kuanzia tarehe ya kuwasilishwa pingamizi hilo.

9. Mtu yeyote au chama cha siasa ambacho hakitaridhika na uamuzi wa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kitawasilisha rufaa kwa Msimamizi wa Uchaguzi ambaye ataishughulikia rufaa hiyo katika muda wa siku tano baada ya kupokea rufaa hiyo.

10. Uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi kuhusu rufaa iliyowasilishwa chini ya Kanuni Ndogo ya (8) ya Kanuni hii utakuwa mwisho.


No comments: