Mwenyekiti Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Hai akizungumza jambo na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, wakiwa jukwaani |
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli jana aliungana na viongozi wenzake wa Serikali kuwamwagia sifa viongozi wa vyama vya upinzani baada ya kumwelezea Mbunge wa Hai na Mwenyekiti Chadema, Freeman Mbowe kuwa ni mpigania maendeleo ya wananchi na kwamba alitakiwa awe malaika.
Dk Magufuli alimuelezea kiongozi huyo wa upinzani
bungeni kuwa ni mtu ambaye anafuatilia maendeleo ya watu bila ya kujali
itikadi zao.
Waziri huyo ameungana na Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kusifu utendaji wa viongozi wa upinzani.
Februari 10, Rais Kikwete alisifu utendaji wa meya
wa Manispaa ya Moshi, Jaffar Michael wa kuwaletea maendeleo wananchi,
na siku 12 baadaye Waziri Pinda alimsifu mbunge wa Iringa Mjini
(Chadema), Mchungaji Peter Msigwa kwa kuwa kiongozi wa kwanza kuchangia
vitanda 30 kwenye Hospitali ya Frelimo.
Jana, Dk Magufuli alimmwagia Mbowe sifa hizo
katika mkutano wa hadhara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya
Kwasadala-Masama-Machame katika Jimbo la Hai inayojengwa kwa kiwango cha
lami.
“(Mbowe)Unadhihirisha kwamba maendeleo hayana
chama na kwa kweli tukienda hivi Tanzania itakuwa ni nchi ya kutolewa
mfano. Sincerely (kwa dhati) nakupongeza Mbowe na Mungu akubariki,”
alisema.
Kabla ya Dk Magufuli kutoa pongezi hizo, Mbowe
aliwataka wanasiasa kutekeleza ahadi zao kwa vitendo kwa kuwa maendeleo
hayana itikadi.
“Mimi naamini maendeleo hayana itikadi. Jambo jema
likifanywa na chama chochote cha siasa ama kiongozi wa chama chochote
au Mtanzania, kama ni jema anastahili kupongezwa,” alisema Mbowe.
“Hakuna aibu ya kukiri pale jambo jema
linapofanyika. Ujenzi wa Barabara ya Kwasadala-Mula-Machame ni jambo
jema,” alisisitiza Mbowe.
Hata hivyo, alitumia mkutano huo wa hadhara
uliofanyika Kijiji cha Masama kumuomba Dk Magufuli atoe maagizo ya
kiserikali baada ya viongozi wawili wa CCM kutishia kuchoma moto greda
lake.
“Nimenunua greda ili tusaidiane na Serikali,
lakini juzi diwani na mwenyekiti wa kijiji walitishia kuchoma moto greda
eti kwa sababu mbunge hajapewa kibali cha kuchimba barabara,”
alilalamika.
Mbowe alisema vyama vya siasa ni lazima vifanye pamoja kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo.
No comments:
Post a Comment