Mhe Godbless Lema |
______________________
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,kwa maslahi ya umma wa Watanzania na watu wa Arusha, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwepo hapa leo, kuwasilisha maoni na mapendekezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2015/2016
Mheshimiwa Spika, familia yangu inatambua kwamba kuwa Mbunge wa Upinzani katika Taifa linalopuuza utu, demokrasia na haki ni adha kubwa kutokana na kuzungukwa na mazingira yaliyojaa vitisho, kejeli, mateso , matusi na kupandikiziwa hofu. Hata hivyo napenda kumshukuru Mke wangu, kwa kuwa amekuwa msaada mkubwa sana kwangu katika dua ,sala na maombi na hivyo kuifanya kazi hii kuwa ya thamani na nyepesi kwangu. Napenda pia kuwapongeza wanangu Allbless na Terrence kwa ucheshi wao unaoifanya familia nzima kuwa na furaha wakati wote.
Mheshimiwa Spika, leo hii natoa pia shukurani zangu za dhati kabisa kwa Wakurugenzi wa Arusha Development Foundation (ArDF) kwani ni jana tu, tarehe 21 Mei 2015 ambapo tumeweza kusaini Mkataba wa kuanza Ujenzi wa Hospitali ya Mama na Mtoto pamoja na Chuo cha Wakunga huko Burka Jijini Arusha. Namshukuru pia Dkt. Alex Browning pamoja na timu yake yote kwa nia ya dhati kabisa ya kukubali na kutafuta fedha ambazo amekwisha zipata kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Mama na Mtoto katika Nchi yetu .
Mheshimiwa Spika , namshukuru pia rafiki yangu, hayati Wakili Nyaga Mawalla kwa mchango wake wa kutoa eneo la ujenzi wa hospitali hiyo. Alikuwa mtu mwema na mwenye kupenda watu na maendeleo, leo hatuko naye wakati kazi hii njema inaanza, lakini mchango wake hautasaulika kwetu Sisi na Jamii ya watu wa Arusha na Tanzania, hususan kwa Afya ya Mama na Mtoto.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kwa wapiga kura wangu wa Jimbo la Arusha Mjini. Ninajua na wanajua kuwa mwaka huu kutakuwa na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Ushindi kwetu ni jambo la kutafakari na uamuzi tumeshafanya tujiandikishe kwa wingi daftari litakapokuja hivi karibuni ili kuthibitisha ushindi usio na hofu. Tumepewa fursa ya mabadiliko kwa kujiandikisha na tutumie wajibu wetu kushawishi ndugu zetu popote walipo ndani ya nchi yetu kujua umuhimu wa jambo hili la uandikishaji kwa ajili ya kuiondo CCM madarakani.
Endelea.....
Mheshimiwa Spika, Kwa kuzingatia maudhui ya methali isemayo ‘Sikio la kufa Halisikii Dawa”, na kwa kuzingatia uhalisia wenyewe kwamba Serikali hii ya awamu ya nne inamaliza muda wake; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kipindi hiki haitatoa tena ushauri kwa kuwa Serikali hii haitakuwepo madarakani tena kuutekeleza ushauri huo, na badala yake tutaonesha jinsi ambavyo Serikali hii ya CCM imeshindwa kutekeleza majukumu yaliyopo chini ya Wizara hii kwa muda wote wa miaka 53 ya Uhuru iliyokaa madarakani; na kutoa mwelekeo wa nchi na masuala muhimu yatakayotekelezwa na Serikali mpya inayotokana na Upinzani baada ya ushindi wa kishindo katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu wa 2015.
HALI YA USALAMA NA AMANI YA NCHI YETU
2.1. Uchochezi wa Kidini na Kikabila
Mheshimiwa Spika, kwa mihula yote miwili ya Utawala wa Serikali hii ya awamu ya nne, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikikemea tabia mbaya na hatari kwa mustakabali wa amani ya nchi ya uchochezi wa kidini na kikabila unaofanywa kwa makusudi na viongozi wa CCM kwa maslahi yao ya kisiasa.
Mheshimiwa Spika, Tatizo la Udini na ukabila limeendelea kuwa hatari kwa ustawi wa amani ya nchi yetu, na hili ni janga kubwa ambalo linaratibiwa na Chama tawala na washirika wake kwa maslahi ya kisiasa. Hivi karibuni tumeshuhudiai Siasa chafu za rushwa, ukabila na udini zikiibuka nyakati hizi za Uchaguzi. Kwa Arusha Mjini, siasa hizi za ukabila zinafanywa na zinaendelea kufanywa na baadhi ya makada wa CCM.
Mheshimiwa Spika, wakati uchochezi huu wa kidini na kikabila unafanyika, Usalama wa Taifa wanajua, Polisi wanajua lakini hawachukui hatua yoyote. Nadhani wanafikiri kwamba ni mkakati mzuri wa ushindi kwa CCM lakini kumbe ni mkakati unao hatarisha hali ya usalama na amani nchini.
Ninawataka hao wanaofanya vikao kwenye mazizi ya ng’ombe kwa misingi ya kikabila na kupanga mikakati ya kutoa rushwa ili kushinda Ubunge katika Jimbo wa Arusha kuacha mara moja kufanya hivyo kwani Arusha itaendelea kuhitaji Mbunge mkakamavu na sio Kiongozi wa Ukoo .
Mheshimiwa Spika, napenda kuwaahdi wapiga kura wangu wa Arusha Mjini kwamba Chama changu na Mimi mwenyewe hatuta fanya Siasa za rushwa za kuwanunua wapiga kura. Hii ni kwa sababu tunatafuta uhuru kamili wa nchi hii, hivyo hatuwezi kujadili bei ya UTU wa mwanadamu.
Mheshimiwa Spika, mwaka jana nileleza katika hotuba yangu kwamba “tatizo la udini na ukabila katika taifa hili linaonekana kuendelea kukomaa, na ni tatizo ambalo halitamwacha hata mmoja wetu salama. Ni tatizo ambalo hakuna mshindi atakayepatikana. Ni tatizo ambalo hata kama litaisambaratisha nchi, hata wale watakaofanikiwa kuikimbia nchi hawatakuwa salama huko wanakokwenda kwa sababu watakuwa bado na imani zao na chuki hiyo dhidi imani nyingine itaendelea popote watakapokuwa”.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hatari inayoweza kutokana na uchochezi wa kidini na kikabila, Kambi Rasmi ya Upinzani iliitaka Serikali kutafakari upya na kuleta sheria mpya itakayokataza na kuwawajibisha kwa nguvu zote wale wote watakaojaribu hata kwa maneno kueneza chuki au ubaguzi dhidi ya dini, kabila au rangi. Lakini mpaka sasa jambo hilo halijafanyika. Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kwa mara nyingine tena kutoa angalizo kwa Serikali kuchukua hatua za dharura za kukabiliana na athari zinazoweza kutokea kutokana na uchochezi wa kidini na kikabila hasa tunapoelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
2.2. Ajali za Barabarani na Usalama wa Wasafiri
Mheshimiwa Spika, katika miaka yote kumi ya utawala wa awamu ya nne ya Serikali hii ya CCM; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiitaka Serikali Kuchukua hatua madhubuti za kupunguza matukio ya ajali barabarani ambayo yamepoteza maisha ya wananchi wengi na kuacha wengine wakiwa walemavu . Jambo la kushangaza na kusikitisha ni kwamba; kadiri tunavyoipa Serikali ushauri mzuri ndivyo inavyozidi kuzembea na ajali zinazidi kuongezeka.
Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu kwa kipindi cha Januari hadi Aprili mwaka huu wa 2015 ambao kimsingi ndio mwaka wa mwisho wa uhudumu wa Serikali hii ya awamu ya nne, ndio vifo vingi vimetokea kutokana na ajali za barabarani kuliko miaka ya nyuma. Kwa mujibu wa Taarifa ya Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kamishna wa Polisi Mohamed Mpinga, “Kuanzia Januari zimetokea ajali 823 vifo 273 majeruhi 876, mwezi Februari zimetokea ajali 641, vifo 236 majeruhi 726 na Machi zimetokea ajali 652, vifo 357 na majeruhi 761”
Mheshimiwa Spika, Kama usafiri wa reli ungeboreshwa na kuwa wa uhakika, na kama pia usafiri wa anga ungeboreshwa kwa kuwa na ndege nyingi na hivyo kufanya gharama za usafiri wa anga kupungua na hivyo kumwezesha mwananchi wa kawaida kuzimudu basi ingesaidia sana kupunguza matumizi ya barabara kwa mabasi ya abiria na malori ambayo kimsingi ndiyo yanaongoza kwa ajali za barabarani. Barabara zingetumika tu kwa magari binafsi na ajali za barabarani zingepungua. Lakini ni aibu kwa taifa kwamba Nchi yenye rasilimali nyingi kama Tanzania bado kusafiri kwa ndege tunaambiwa ni ndoto kama kauli mbiu ya Fast jet inavyosema “ Flying your dream”
Mheshimiwa Spika, Polisi wamekuwa wepesi kuwatupia madereva lawama kuwa ni wazembe kila inapotokea ajali. Lakini wanasahau kuwa ajali nyingine zinatokea kutokana na miundo mbinu mibovu, na pia ajali nyingine zinasababishwa na polisi wa usalama barabarani wenyewe kwa kupokea rushwa na kuyaruhusu magari mabovu kuendelea na safari. Aidha, utaratibu wa sasa wa kumtaka askari wa usalama barabarani kukamata makosa yasiyopungua thelathini kwa siku na kuyaandikia “notification”na kukusanya faini ya shilingi 30,000/= kwa kila kosa kumekifanya kikosi cha usalama barabarani kuwa kama kitengo cha TRA kwa kukusanya mapato. Inasikitisha kusikia Jeshi la polisi likisifiwa kwa ukusanyaji wa mapato bila kujali athari zilizotokea baada ya ukusanyaji wa mapato hayo.
Mheshimiwa Spika, hatutaweza kuondoa ajali barabarani kwa kuongeza faini, isipokuwa kwa kuboresha miundombinu mingine ya usafirishaji kama vile reli na usafiri wa anga ili kupunguza matumizi ya barabara.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuwaahidi wananchi kwamba endapo Upinzani utaunda Serikali baada ya Uchaguzi wa Oktoba mwaka huu, suala la usalama barabarani litakuwa ni mojawapo ya vipaumbele vya kazi za Serikali kwa kuwa watanzania wamechoka kusikia habari za mauti na ulemavu unaosababishwa na matumizi mabaya ya barabara. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawasihi Wananchi wote kuwa makini na matumizi ya barabara hasa wale waendesha boda boda , kwani matumizi barabara yasiozingatia sheria za barabarani yanayofanywa na wananchi ni chanzo kikubwa cha ajali barabarani pia .
UKOMESHAJI WA MATUMIZI NA BIASHARA HARAMU YA DAWA ZA KULEVYA NCHINI
Mheshimiwa Spika, kwa miaka yote kumi ya utawala wa Serikali hii ya CCM, Kambi Rasmi ya Upinzani ilipiga sana kelele kuhusu wimbi kubwa la matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya nchini lilivyokuwa linazidi kuangamiza nguvu kazi ya taifa. Licha ya Serikali hii ya CCM kupitia Rais Jakaya Kikwete kukiri kwamba inawafahamu kwa majina wanaohusika na biashara hiyo, bado hakuna hatua za wazi zilizochukuliwa dhidi ya wahusika hao.
Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya CCM inaweza kujitetea kwamba ina mkakati wa kukomesha biashara haramu ya dawa za kulevya na ndio maana ikaleta Bungeni Muswada wa Sheria ya Udhibiti na Usimamizi wa Dawa za Kulevya ya mwaka 2014 uliojadiliwa na kupitishwa na Bunge katika Mkutano wa Bunge uliopita. Lakini katika maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu muswada wa sheria hiyo tulionesha jinsi ambavyo sheria hiyo haiwezi kudhibiti biashara haramu ya dawa za kulevya: Sababu za kusema hivyo zilikuwa ni kama ifuatavyo: nanukuu:
Adhabu kali sana zilizotajwa katika muswada huu, zinaweza kuvutia mazingira ya rushwa hususan katika vyombo vilivyopewa mamlaka ya upekuzi na ukamataji wa watuhumiwa wa dawa za kulevya na pia katika mahakama zetu.
Mheshimiwa Spika, ni vema kutambua kwamba biashara hii ya dawa za kulevya ni biashara ya fedha nyingi na mara nyingi wahusika ni matajiri. Hivyo ikiwa mtuhumiwa amekamatwa; na kwa mujibu wa makosa yake anajua kwamba anakabiliwa na kifungo cha miaka 30 gerezani au faini ya shilingi milioni 200, yuko radhi kutoa hata milioni 50 kwa afisa aliyemkamata ili asimfikishe kwenye vyombo vya sheria. Na kwa jinsi hali ya maisha ya watumishi wa umma ilivyo duni, ni jaribu kubwa sana kwa afisa mkamataji kukataa shilingi milioni 50 aliyopewa kama rushwa ili asimfikishe mtuhumiwa mahakamani.
Katika mazingira ya rushwa vilevile, mahakimu wanaweza kutoa adhabu za faini pekee bila kifungo kwa watuhumiwa wa dawa za kulevya watakaopatikana na hatia chini vya masharti ya sheria inayopendekezwa, jambo ambalo linaweza kusababisha biashara ya dawa za kulevya kuendelea kushamiri na kukomaa hapa nchini. Hii ni kwa sababu wafanya biashara wa dawa za kulevya wana uwezo wa kifedha wa kulipa faini hizo bila ugumu wowote.
Kuendelea kutoza faini kwa mtu anayepatikana na hatia ya kujihusisha na dawa za kulevya, ni sawa na kuhalalisha biashara hiyo kwani ni sawa na mfanya biashara kulipia kodi au ushuru wa biashara yake.
Serikali kukubali kupokea faini na kumwachia mtu aliyepatikana na hatia ya kujishughulisha na baiashara ya dawa za kulevya, haina tofauti na kupokea rushwa (iliyogeuzwa jina na kuitwa faini) ili kumwachia mfanyabiashara wa dawa za kulevya kuendelea kuangamiza kizazi cha taifa hili.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani iliendelea kuonesha wasiwasi wake juu ya uwezo wa sheria hiyo, kukomesha biashara ya dawa za kulevya hapa nchini kwa sababu Tanzania ilikuwa na Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya ya Mwaka 1995, tumekuwa na Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, tumekuwa na Polisi miaka yote lakini viwango vya uingizaji na usafirishaji wa dawa za kulevya vimekuwa vikiongezeka. Kwa uhalisia huu ni dhahiri kwamba; tatizo sio sheria bali ni kukosekana kwa utashi wa Serikali kushughulikia jambo hilo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali hii ya CCM ya awamu ya nne imeshindwa kukomesha matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya, na kwa kuwa imejulikana sasa kuwa Serikali haina Mpango Kabambe wa kukomesha biashara haramu ya dawa za kulevya hapa nchini, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawaahidi wananchi kwamba; endapo vyama vya upinzani vitafanikiwa kushinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015 na kuunda Serikali, vita dhidi ya matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya nchini itakuwa ni kipaumbele katika kazi za Serikali.
UUNDWAJI WA TUME YA UCHUNGUZI WA KIMAHAKAMA (THE JUDICIAL INQUEST COMMISION) KUCHUNGUZA MAUAJI YA RAIA YALIYOFANYWA NA VYOMBO VYA DOLA
Mheshimiwa Spika, kwa miaka yote kumi ya utawala wa Serikali hii ya awamu ya nne, Kambi Rasmi ya Upinzani ilikuwa ikipiga kelele na kulaani sana mauaji ya raia wasio na hatia yanayofanywa na vyombo vya dola hususan Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Spika Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, iliitaka Serikali kuunda Tume ya Uchunguzi wa Kimahakama au kwa lugha nyingine Mahakama ya Korona kwa ajili ya kuchunguza vifo vinavyotokana na mateso yanayofanywa na jeshi la Polisi, kwa mujibu wa sheria ya kuchuguza vifo vyenye utata (The Inquest Act) lakini mpaka sasa hivi Serikali haijafanya hivyo licha ya Waziri Mkuu kuahidi hapa Bungeni mara kadhaa kwamba Serikali ingeunda tume hiyo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutambua kwamba kumwaga damu isiyo na hatia katika nchi ni laana katika nchi. Hivyo, Serikali iliepushe taifa na laana kwa kuzuia umwagaji damu ya watu wasio na hatia.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali hii ya CCM haioni umuhimu wa kuunda Tume ya Kimahakama , Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuwahakikishia wananchi wote kwamba; endapo upinzani utashinda na kutwaa madaraka ya dola, utakuwa ndio mwisho wa uonevu unaofanywa na vyombo vya dola dhidi ya raia na zaidi sana hakutakuwa na ya damu ya raia wa nchi hii itakayopotea bure kwa sababu ya uonevu. Hata hivyo tunawapa pole wote ambao ndugu zao wamefikwa na mauti na kwamba huzuni yao na uchungu wao unapewa thamani na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
UBORESHAJI WA BAJETI YA JESHI LA ZIMA MOTO NA UOKOAJI
Mheshimiwa Spika, katika hotuba zote za Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu bajeti ya Wizara hii, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiitaka Serikali kuongeza fedha za miradi ya maendeleo katika wizara hii kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya zima moto na uokoaji kwa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji lakini Serikali haijatilia maanani suala hili.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba yetu ya mwaka jana tulieleza; na ninakukuu:
“Kwa mujibu wa Randama ya Jeshi la Zimamoto, fungu 14 (uk. 2) katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/14 hakuna fedha yoyote iliyotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa Jeshi la Zima Moto.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Randama hiyo, huu ni mwaka wa tatu mfululizo kwa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji kutotengewa fedha kwa ajili ya miradi ya Maendeleo. Kutokana na hali hiyo, Jeshi hilo limeshindwa kuendeleza ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makao Makuu – TAZARA, Dar es Salaam, kushindwa kukarabati na kujenga vituo vipya vya zimamoto, kushindwa kununua vitendea kazi mbalimbali ikiwemo vifaa vya maokozi na vifaa vya kuzimia moto.
Mheshimiwa Spika,
Sote ni mashahidi wa majanga ya moto, maghorofa kuporomoka, meli kuzama, mafuriko na kila aina ya majanga ambapo idara ya zima moto imekuwa ikishindwa kufanya chochote na hivyo kuwaacha wananchi wakiangamia katika majanga hayo. Kambi Rasmi ya Upinzani inashawishika kuamini kwamba Serikali haina nia njema na usalama wa raia na ndio maana haitengi fedha hata senti moja katika miradi ya maendeleo ya Jeshi la Zima Moto. Kama Serikali haioni umuhimu wa Jeshi la Zima Moto ni bora kulifuta kuliko kuliacha wakati hailiwezeshi kufanya kazi yake”.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaungana na wananchi wote waliopata madhila kutokana na majanga mbalimbali ambapo Jeshi la Zima Moto na Uokoaji lilishindwa kuwapatia msaada kutokana na kukosa vifaa vya kutendea kazi. Aidha, tunawaahidi wananchi kwamba endapo tutaingia madarakani, bajeti ya Jeshil la Zima Moto na Uokoaji itaboreshwa ili Jeshi hilo liweze kufanya kazi kwa ufanisi ili kuwaokoa wananchi wakati wa majanga.
HATIMA YA VITAMBULISHO VYA TAIFA
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ikiitaka Serikali kutoa ukomo wa muda, ambapo kila raia wa Tanzania atapatiwa Kitambulisho chake cha Taifa na kuainisha gharama zilizotumika katika mchakato mzima wa kutengeneza vitambulisho vya Taifa.
Mheshimiwa Spika, inasikitisha sana kuona kwamba tangu mchakato huo uanze, Serikali haitoi mrejesho wa namna zoezi hilo linavyoendelea, ni wananchi wangapi wameshapata vitambulisho hivyo, ni lini kila raia wa Tanzania atakuwa amepatiwa kitambulisho chake cha Taifa, na ni fedha kiasi gani zimetumika hadi sasa katika mchakato huo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa serikali hii ya awamu ya nne inaondoka madarakani kabla haijakamilisha mchakato wa kuwapatia wananchi wote vitambulisho vya taifa, na kwa kuwa fedha nyingi za walipa kodi zimetumika kuanzisha mchakato huo, Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuwaahidi wananchi kwamba tutakapoingia madarakani katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2015 na kuingia madarakani, zoezi hilo litakamilishwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
MABORESHO YA MAZINGIRA NA AFYA ZA MAHABUSU NA WAFUNGWA MAGEREZANI
Mheshimiwa Spika, kwa miaka yote ya utawala wa Serikali ya awamu ya nne, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiitaka Serikali kuchukua hatua ya kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu Magerezaji sambamba na kuboresha lishe na huduma za afya kwa Wafungwa na Mahabusu.
Mheshimwia Spika, licha ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuishauri Serikali mara zote hizo, msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani umeendelea kuwa ni tatizo, hali kadhalika huduma za afya na lishe kwa mahabusu na wafungwa zimeendelea kuwa duni.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali hii imeshindwa kupunguza msongamano wa mahabusu na wafungwa magerezani kwa kubuni adhabu mbadala za nje kwa makosa madogomadogo badala ya vifungo, na kwa kuwa Serikali hii imeshindwa pia kufanya upelelezi wa kesi zinazowakabili watuhumiwa wa makosa mbalimbali kwa wakati na hivyo kusababisha msongamano wa mahabusu magerezani ambapo hawazalishi chochote isipokuwa wanaitia hasara Serikali kwa kula bila kufanya kazi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuwaahidi wananchi wote kwamba, endapo Upinzani utaingia madarakani msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani utapunguzwa kwa kutoa adhabu mbadala ya vifungo vya nje kwa makosa madogo madogo, na kukamilisha upelelezi za kesi mbalimbali kwa wakati ili pia kupunguza msongamano wa mahabusu.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni pia inalitaka Jeshi la Polisi kuwa linakamata na kuwatia Watu mahabusu wakati uchunguzi wa kina ukiwa umeshafanyika tofauti na sasa ambapo mtu anayehisiwa tu kuwa ni mhalifu anaweza kuwekwa mahabusu na kukaa huko hadi miaka zaidi ya mitano na baadae kuambiwa kuwa hana hatia, huu ni uvunjaji wa haki za Binadamu.
UBORESHAJI WA MAZINGIRA YA KAZI KWA ASKARI MAGEREZA.
Mheshimiwa Spika, kwa mihula yote miwili ya utawala wa Serikali hii ya awamu ya nne, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiitaka Serikali kujenga nyumba za Askari wa Magereza ili kuboresha mazingira yao ya kazi . Aidha, Kambi Rasmi ya iliitaka Serikali hii kuondoa urasimu na utaratibu kandamizi katika Jeshi la Magereza kuhusu Mpango wa kujiendeleza kielimu kwa maafisa wa Magereza ambapo utaratibu huo ulikuwa unakwenda kinyume na General Service Order (GSO) na sheria nyingine za kazi.
Mheshimiwa Spika, tatizo la msingi kuhusu kujiendeleza kielimu kwa maafisa wa magereza lilikuwa ni muda wa kisheria wa miaka miwli ya kukaa kwenye kituo cha kazi baada ya kuajiriwa kwa mara ya kwanza (first appointment) kabla ya kuomba ruhusa ya kujiendeleza kimasomo kukiukwa na badala yake waombaji wa nafasi za kujiendeleza kielimu kutakiwa kukaa kwenye kituo cha kazi hadi miaka sita ndipo waruhusiwe kujiendeleza kielimu.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba mazingira bora ya kazi, na maendeleo ya rasilimali watu ni nyenzo muhumu ya utendaji kazi kwa ufanisi si kwa Jeshi la Magereza tu bali kwa sekta na taasisi mbalimbali za Serikali zinazojali weledi na tija kwa watumishi wake. Kwa minajili hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inapenda kuwaahidi askari Magereza kwamba iko nao bega kwa bega kukabiliana na changamoto zinazowakabili, na kwa maana hiyo iwapo upinzani utachukua madaraka ya nchi, sera ya maendeleo ya rasilimali watu kwa askari wa Jeshi la Polisi itaboreshwa ili kutoa fursa nyingi zaidi za kujiendeleza kielimu kwa maafisa wa Jeshi la Polisi na Magereza, na halikadhalika mazingira ya kazi kwa Askari wa Jeshi la Polisi na Magereza ikiwa ni pamoja na kuwajengea nyumba nzuri zenye staha yataboreshwa.
MABORESHO YA POSHO YA CHAKULA (RATION ALLOWANCE) KWA JESHI LA POLISI
Mheshimiwa Spika, kufuatia ugumu wa maisha ya Askari wetu wa Jeshi la Polisi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kwa miaka yote ya utawala wa Serikali ya awamu ya nne, imekuwa ikiitaka Serikali, kuongeza posho ya chakula (Ration allowance) kwa askari wa Jeshi la Polisi ili walau posho hiyo ishabihiane na posho ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili waweze kukabiliana na ugumu wa maisha. Kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za bunge (hansard) Waziri wa Fedha wa wakati huo Marehemu William Mgimwa alikubali posho ya chakula ya shilingi 225,000/= kwa mwezi sawa na shilingi 7,500/= kwa siku kwa kila askari. Taarifa tulizo nazo ni kwamba posho hiyo haijalipwa mpaka leo, licha ya Serikali kuahidi kuwalipa posho hiyo.
Mheshimiwa Spika, katika mazingira kama haya ambapo Serikali inaahidi ndani ya Bunge hili kupandisha posho za chakula za askari Polisi halafu haitekelezi, inataka tuishauri nini tena?
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hoja ya kupandisha “ration allowance” kwa askari wetu wa Jeshi la Polisi ilianzishwa na Kambi ya Upinzani, na kwa kuwa kwa miaka yote ya utawala wa Serikali ya awamu ya nne Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiwatetea askari wa Jeshi la Polisi ili walipwe posho ya chakula ya shilingi 7,500/= kwa siku kwa kila askari; na kwa kuwa kwa mihula yote miwili ya utawala wa Serikali ya awamu ya nne, Serikali imeshindwa kutekeleza ahdadi yake yenyewe iliyoitoa hapa Bungeni kwamba ingepandisha posho hiyo, hivyo basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuchukua nafasi hii kuwaahidi Askari wote waliopo chini ya Jeshi la Polisi kwamba endapo Upinzani utaunda Serikali baada ya ushindi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2015, posho hiyo itapandishwa haraka iwezekanavyo kwa kuwa ni sera ya Upinzani kuboresha maslahi ya askari wa Jeshi la Polisi. Ili kutimiza azma hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalitaka Jeshi la Polisi Nchini kukataa kutumika kiasiasa na Serikali ya CCM kuukandamiza upinzani na badala yake wafanye kwazi kwa kuzingatia sheria na taratibu zinazotumika kuongoza utendaji wa Jeshi hilo.
UDHIBITI WA FUJO NA MAUAJI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU WA 2015.
Mheshimiwa Spika, kwa miaka yote kumi ya utawala wa Serikali hii ya awamu ya nne, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipigia kelele sana na kulaani mauaji ya raia yenye sura ya kisiasa. Tulisema mauaji haya yana sura ya kisiasa kwa sababu waliouwawa ni viongozi wa vyama vya siasa vya Upinzani na mauaji hayo yalitokea vipindi vya chaguzi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, Itakumbukwa kwamba katika Uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Igunga aliuwawa kiongozi wa CHADEMA aliyejulikana kwa jina la Mbwana Masoud, na pia aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo, naye aliuwawa na watu wasiojulikana mara baada ya Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa pia kwamba wabunge wa CHADEMA, Mhe. Highness Kiwia wa Jimbo la Ilemela na Mhe. Salvatory Machemuli wa Jimbo la Ukerewe walinusurika kifo baada ya kujeruhiwa vibaya kwa mapanga na watu wanaosakiwa kutumwa na viongozi wa CCM mkoani mwanza. Inasikitisha kwamba shambulio hilo dhidi ya wabunge hao lilitokea mbele ya maafisa wa polisi ambao hawakusaidia chochote.
Mheshimiwa Spika nimelazimika kukumbusha masuala haya ili Serikali ijipange vizuri na kuliagiza Jeshi la Polisi kuwalinda raia, wafuasi wa vyama vya siasa, wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kwa haki na usawa hasa katika kipindi hiki ambapo taifa linaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu. Endapo Jeshi la Polisi litaendelea kutumika kisiasa, na kuwaacha “green guards” wa CCM kufanya fujo kwenye mikutano ya kampeni ya vyama vya Upinzani, basi vyama vya Upinzani vitalazimika kuchukua jukumu la kujilinda vyenyewe.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya vyama vya siasa vinavyounda UKAWA, napenda kutoa tahadhari kwa CCM kwamba, endapo wamepanga njama zozote zile kuhujumu vyama vya UKAWA katika uchaguzi Mkuu wa Okotoba, 2015, njama hizo zitadhibitiwa ipasavyo. Napenda kuwahakikishia CCM kwamba Upinzani wa sasa hivi una nguvu kuliko wakati mwingine wowote, hivyo wasijaribu!!!
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa taifa linaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, na kwa kuwa kipindi cha uchaguzi ni kipindi ambacho amani ya nchi yetu inatakiwa kulindwa kwa nguvu zaidi kuliko vipindi vingine; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kutoa angalizo kwa Serikali kuhusu mambo mawili muhimu ili kunusuru amani ya nchi yetu kuelekea Uchaguzi Mkuu. Masuala hayo ni kama ifuatavyo:
Kutochezea Haki ya Mwananchi Kujiandikisha kuwa Mpiga Kura:
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kurudia na kusisitiza tena kwamba mzaha katika jambo hili hautavumilika kwani haki haiombwi, inadaiwa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura ili waweze kuamua nani atakuwa kiongozi wao kwenye uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamkumbusha kila mwananchi atambue kwamba “Kura yako ni Maisha yako, Nenda Kajiandikishe Sasa”
Kutofanya Mzaha na Uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi:
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudia tena kuionya Serikali kutofanya mzaha na jambo hili kwani linaweza kuiingiza nchi katika machafuko makubwa. Napenda kurudia tena rai yetu kwa Serikali: “Tunataka Tume Huru ya Uchaguzi, si kwa sababu tunataka kushinda uchaguzi bali ni kwa sababu tunataka kulinda Imani ya Mpiga Kura ili kulinda amani ya nchi yetu”.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.
Godbless Jonathan Lema (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI NA
WAZIRI KIVULI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI
Godbless Jonathan Lema (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI NA
WAZIRI KIVULI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI
No comments:
Post a Comment