Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Mh Salum Mwalim akihutubia Mkutano wa adhara katika kata ya Endasaki Wilayani Hanang . |
Wakati uamuzi wa Serikali kukusudia kuwasilisha bungeni miswada
mwili kwa ajili ya kutunga sheria za Huduma ya Vyombo vya Habari na Haki ya Kupata Taarifa ukiendelea
kupingwa, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Zanzibar, Salum Mwalim ameenda mbali na kuwashauri Wamiliki wa Vyombo vya
Habari (MOAT) kususia habari taarifa za serikali kwa wiki moja.
Akizungumza jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Endasaki,
Hanang, mkoani Manyara, Mwalim alisema kuwa MOAT wanapaswa kuacha kutoa taarifa
zinazoihusu Serikali akisema kuwa hiyo ni mojawapo ya njia za kuonesha hisia
zao dhidi ya kile alichodai kuwa ni njama za serikali kwa vyombo vya habari na
wanahabari.
Mwalim ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari alisema kuwa
anaungana na wadau wa vyombo vya habari nchini wakiwemo wamiliki na Baraza la
Habari nchini (MCT) katika kupinga miswada hiyo, hususan ule wa Huduma ya
Vyombo vya Habari ambao umeelezwa kuwa na vipengele vinavyolenga kuminya uhuru
wa habari na upatikanaji wa taarifa kwa vyombo vya habari na wananchi wa
kawaida.
“Naomba kuungana na wanahabari wenzangu na Watanzania wote kwa
ujumla kuupinga muswada huu unaolenga kuminya na kukandamiza uhuru wa habari si
kwa vyombo vya habari pekee bali mwananchi mmoja mmoja katika haki ya kupata
taarifa.
“Naungana na wamiliki wa vyombo vya habari na Baraza la Habari
nchini kwa uamuzi wao wa kuupinga vikali na kuamua kutuma timu ya watu kwenda
Dodoma kuzungumza na wabunge ambao hawako tayari kuona nchi inakuwa na sheria
zinazoturudisha nyuma badala ya kusonga mbele pamoja na mataifa mengine
yanayoendelea kwa sababu ya kuheshimu uhuru wa habari na wananchi kupata
taarifa.
“Badala ya serikali kupeleka muswada ambao utapitishwa na kuwa
sheria yenye maslahi kwa na nia njema kwa wamiliki wa vyombo vya habari,
wanataaluma na taaluma yenyewe ya habari, inafikiria namna ya kuminya hata
uhuru huu mdogo uliopo sasa ambao nao tumekuwa tukiulalamikia kwa sababu ya
kuwepo kwa sheria kandamizi kama ile ya Magazeti, Usalama wa Taifa na zingine,”
alisem Mwalim na kuongeza;
“Nawashauri MOAT ili serikali hii ielewe kuwa suala hili si la
mzaha, waache kutoa taarifa zinazoihusu serikali hii ya CCM kwa muda wa wiki
moja ili kuelezea hisia zao kuwa hawakubaliani kabisa na njama za kuminya uhuru
wa habari.”
Kiongozi huyo ambaye alizindua mafunzo ya uzalendo kwa vijana wa
chama hicho wilayani Hanang akiendelea na ziara ya chama hicho katika
kuhamasisha wananchi kujiandikisha kwa wingi kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga
Kura na kujiandaa kwa Uchaguzi Mkuu, Oktoba mwaka huu, alidai kuwa kuminya
uhuru wa habari na upatikanaji wa taarifa hutokana na hofu ya watawala
kuondolewa madarakani.
Alisema kuwa wakulima wanapokuwa na shida ni vyombo vya habari
ambavyo huwasemea hivyo hivyo kwa makundi mengine katika jamii kama wafugaji,
walimu, madktari, wanafunzi, hivyo akavitaka vyombo vya habari na wanahabari
nao kuchukua hatua ngumu za kujisaidia na kuokoa taaluma yao.
Alisema kipengele kinachotaka vyombo vya habari vya binafsi kuungana
na Shirika la Utangazaji la Taifa ni kulirudisha nyuma taifa na kukaribisha
udikteta usioweza kuvumilika. Soma Zaidi........
Aliwataka Watanzania kuona kuwa suala hili ni muhimu kwao wala
halihusu watu wachache pekee kwani kunyamaza kimya kutasababisha watawala
kutunga sheria ambayo itawalazimisha wananchi wote kutazama TBC hata kama
hawataki.
Mwalim alikwenda mbali na kusema kuwa kipengele hicho ni cha
ajabu kwa sababu kwa ufahamu wake, hata viongozi wa serikali wenyewe wakiwemo
mawaziri hawaiamini TBC ambapo aliongeza kuwa uzoefu unaonesha wanapokuwa na
mikutano na waandishi wa habari kisha ikawepo TBC pekee huwa hawaendelei hadi
vyombo vya habari vingine viwepo.
Aliwataka Watanzania kupinga muswada huo akisisitiza kuwa vyombo
vya habari ni mhimili wa nne unaojitegemea ambao unapaswa kuwa huru kadri
inavyotakiwa ili kuiangalia mihimili mingine mitatu ya serikali.
Kiongozi huyo anaendelea na ziara yake ambapo leo Ijumaa, kesho
Jumamosi na Jumapili atakuwa katika Mkoa wa Kilimanjaro ambako anatarajiwa
kufanya vikao vya ndani, kuwa mgeni rasmi mahafali Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo
Vikuu wa CHADEMA (CHASO) Mkoa wa Kilimanjaro na kufanya mikutano ya hadhara
No comments:
Post a Comment